Chui Wazidi Kudorora Huku Gor Wakiambulia Sare

Sport Pesa Premier League: Ingwe wadhalilishwa kwenye Derby ya Kataluhya Huku Posta Rangers Wakiwakaba Koo Gor Mahia
 
     Na Wilma Mmbone
   AFC Leopards walidhalalishwa na kushushwa hadhi walipotitigwa magoli 4-1 mikononi mwa Kakamega Homeboyz kwenye mchuano wao wa raundi ya 22 kwenye ligi kuu ya KPL , mchuano uliosakatwa katika uga wa Mumias Complex siku ya Jumapili.
   Andrew Kulecho aliwaweka wenyeji Homeboyz kifua mbele mnamo dakika ya tano kabla ya Sunday Mutuku kuongeza la pili dakika nane baadaye. Andrew Murunga alitikisa wavu wa ingwe mnamo dakika ya 28 na kuwafanya Homeboyz kumiliki kipindi cha kwanza cha mchezo.Kocha wa AFC Leopards Ivan Minnaert alimpumzisha Paul Kiongera huku mfungaji bora katika klabu hiyo Kepha Aswani akichukua nafasi yake. 
   Aswani aliifungia Ingwe bao la kuliwaza moyo katika dakika ya 44 ila furaha ya ingwe ilizimwa na mchezaji Eugene Ambulwa aliyejifunga na kuwazawadi Homeboyz goli la nne na la ushindi kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika. AFC Leopards sasa wameteremka hadi nafasi ya kumi kwenye jedwali na alama 28 huku Homeboyz wakipanda hadi nafasi ya nne na alama 33.
 

Wachezaji wa Kakamega Homeboyz wakisherehekea ushindi dhidi ya Leopards. 
   Kwengineko Gor Mahia waliandikisha sare ya tatu mfululizo hii ni baada ya Posta Rangers kuwakaba koo na kuhakikisha wameishia sare ya kutofungana. K’ogalo walionyesha hamu ya kutaka alama tatu kwenye mtanange huo kwa kumiliki mchuano wote ila ulinzi wa Posta Rangers uliimarika na kuhakikisha kuwa makali ya Gor Mahia hayapenyezi lango lao.

   Gor mahia aidha wanasalia katika nafasi ya pili kwenye jedwali na pointi 37 pointi nne nyuma ya viongozi Tusker. Posta Rangers wanamiliki nafasi ya tisa na pointi 29.


Share on Google Plus

Kuhusu Unknown

Michezo Kenya Tunapenda Spoti

0 comments:

Post a Comment