Kenya yashangaza dunia kwa kutwaa ubingwa Singapore

Na Dan Ogega
Kenya imeandikisha historia kwa kushinda msururu wa Singapore kwa mchezo wa raga kwa wachezaji saba kila upande. Shujaa iliilaza Fiji kwa alama 30-7 na kutwaa taji hilo ambalo lililkuwa likiandaliwa kwa mara ya kwanza katika kalenda ya IRB Circuit Series katika uwanja wa National Stadium.
Tangu mwaka 2008 Kenya ilikuwa imefika awamu ya fainali ya kombe kuu mara mbili kabla ya msimu wa mwaka 2008/2009 ikiwa ni mjini Adelaide mwaka huo na msimu wa mwaka 2012/2013 mjini Wellington. Sasa Kenya ndio taifa la kipekee isipokuwa Afrika Kusini ambalo limeonja ushindi wa angalau msururu mmoja msimu huu.
“Ni hisia nzuri kutwa ubingwa hasa baada ya kutia bidii na kufikia kiwango hiki,” alinukuliwa kiranja wa Shujaa Andrew Amonde.
Mchezaji veterani aliyetwaa tuzo la mchezaji bora katika fainali Collins Injera, alifunga ‘tries’ mbili huku Oscar Ayodi, Samuel Oliech, Nelson Oyoo na Frank Wanyama wakiongeza ‘try’ moja kila mmoja huku Kenya ikiivyoga Fiji na kutamalaki pambano hilo la fainali
Sasa Injera amebakiza ‘tries’ tano ili kumfikia muajentina Santiago Gomez Cora ambaye ni wa kwanza kwenye chati ya wafungaji bora katika mashindano hayo ambaye hadi sasa ana ‘tries’ 230.
“Tumekuwa tukijiandaa vilivyo kwa ajili ya dimba hili na ninaipa heko safu yetun ya ulinzi kwa kuimarika kwa kiasi,” aliongeza Injera.
“Chipukizi pia wamejikakamua na kuendelea kujiboresha kila uchao.”
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Shujaa kutinga fainali msimu huu na mara yao ya tatu katika msururu wa World Sevens Series.
0 comments:
Post a Comment